Watawala wa Marekani waendelea kuunga mkono ghasia za karibuni nchini Iran
Marekani katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo imezidisha uhasama wake dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran na inatekeleza mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Tehran ili eti kuilazimisha ikubali matakwa yake.
Kuhusiana na suala hilo, Washington imekuwa ikitumia kila fursa kuingilia masuala ya ndani ya Iran kwa kisingizio cha kuwahurumia watu wa taifa hili. Baada ya White House na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kutoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Iran, sasa imefika zamu ya Mike Pence Makamu wa Rais Donald Trump kutoa matamshi yasiyo na msingi, eti ya kuunga mkono watu wa Iran. Kupitia ujumbe wa Twitter alioundika siku ya Alkhamisi Alfajiri tarehe 21 Novemba, Mike Pence alitoa madai yasiyo na msingi kuhusiana na machafuko yaliyoshuhudiwa karibuni katika miji kadhaa hapa nchini kwa kusema: Ujumbe wa Marekani uko wazi; Watu wa Marekani wamesimama bega kwa bega na watu wa Iran.
Makamu huyo wa rais wa Marekani ametoa madai hayo katika hali ambayo vikwazo vya kidhalimu na vya upande mmoja vya nchi hiyo ambavyo vinajumuisha bidhaa za msingi yakiwemo madawa na suhula nyingine za tiba, vimewasababishia wananchi wa Iran matatizo makubwa. Kwa mujibu wa wataalamu, watawala wa Marekani si wakweli wanapotoa matamshi ya eti kuwaunga mkono wananchi wa Iran bali ndio wanaowasababishia moja kwa moja matatizo ya kiuchumi ya hivi sasa.
Siku chache kabla ya hapo, Mike Pompeo, Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani pia alikuwa ametoa matamshi ya kuunga mkono ghasia na machafuko ya hivi karibuni hapa nchini na kutaka yadumishwe na wahuni wanaoungwa mkono na nchi za kigeni zikiongozwa na Marekani yenyewe. Akizungumza japo siku ya Jumatano tarehe 20 Novemba katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa shirika la Nato, Pompeo alisema: Mfumo wa kithamani wa Russia, China na Iran unatofautiana na sisi na unaenda kinyume na mfumo wetu.
Washinton inatoa madai ya kutetea na kuunga mkono taifa la Iran katika hali ambayo Trump ametoa matamshi chungu nzima ya dharau na kulikosea heshima taifa hili kwa kulituhumu kuwa ni taifa la kigaidi na kuliwekea vikwazo vya kila aina. Sarah Leah Whitson, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini alisema siku ya Jumatano: Iwapo kweli Mike Pompeo anataka kuwasaidia watu wa Iran, anaweza kufanya hivyo kwa kuondoa vikwazo ambavyo vimeharibu uchumi na usalama wa watu wa Iran.
Machafuko ya hivi karibuni ambayo yalianza Ijumaa tarehe 15 Novemba kwa kisingizio cha kulalamikia nyongeza ya bei ya mafuta ya petroli, kwa mtazamo wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, ilikuwa fursa nzuri ya kuingilia mambo ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hivyo, si tu kwamba ziliamua kuwachochea wahuni waliosababisha hasara na vifo vya watu wasio na hatia bali zilifanya juhudi kubwa za kuishinikiza serikali ya Iran ili eti isikabiliane na majangili hao waharibifu. Ushahidi unaonyesha wazi kuwa nchi za Magharibi zimepanga njama kabambe za kuendesha na kusimamia machafuko na ghasia nchini Iran na ukubwa wa kuharibiwa mali za umma na za watu binafsi katika ghasia za hivi karibuni unathibitisha wazi suala hilo.
Ukubwa wa uharibifu huo unaonyesha wazi kwamba hilo si jambo lililopangwa na watu wa kawaida bali ni vitendo vilivyoratibiwa kwa njia maalumu na nchi za kigeni. Marekani pia kutona na uadui na uhasama ilionao dhidi ya Iran si tu kwamba ilichangia pakubwa kuchochea ghasia hizo bali imetaka kuzidishwa mashinikizo dhidi ya Iran. Bryan Hook, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran, huku akitoa madai ya kukaririwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa matamshi ya uingiliaji wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya Iran kwa kusema kuwa Marekani inaunga mkono moja kwa moja ghasia na machafuko nchini hapa. Kuhusu suala hilo, akizungumza siku ya Jumanne tarehe 19 Novemba mbele ya hadhara ya watengenezaji bidhaa, waajiri na wanaojishughulisha na masuala ya viwanda, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa machafuko ya hivi karibuni nchini yalichochewa na maadui na kusisitiza kuwa hayakuwa ya watu wa kawaida.
Kwa mtazamo wa Iran, serikali ya Trump inatumia vibaya hali ya hivi sasa nchini kwa madhumuni ya kufikia malengo yake maovu na wala haina nia yoyote nzuri na Wairani. Misimamo ya hivi karibuni ya watawala wa Marekani pia inathibitisha wazi uingiliaji wao wa mambo ya ndani ya Iran, suala ambalo linaenda kinyume kabisa na misingi pamoja na sheria za kimataifa na za Umoja wa Mataifa.