Iran: Wanaounga mkono siasa zisizo na hekima katika eneo wanapaswa kuwajibika
(last modified Thu, 12 Dec 2019 02:18:47 GMT )
Dec 12, 2019 02:18 UTC
  • Iran: Wanaounga mkono siasa zisizo na hekima katika eneo wanapaswa kuwajibika

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali taarifa ya kikao cha 40 cha wakuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, waungaji mkono wa siasa zisizo na hekima katika eneo hili la Mashariki ya Kati wanapaswa kutoa majibu na kuwajibika mbele ya fikra za waliowengi.

Sayyid Abbas Mousavi ameongeza kuwa, nchi chache zinazounga mkono kuendelea siasa za sasa zisizo na busara wala hekima katika eneo hili zinapaswa kutoa majibu kwa fikra za waliowengi kwamba, zimefanya nini mbali na kuanzisha kuimarisha makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Iraq, Syria na Yemen na kufungua mlango kwa ajili ya madola ajinabi katika Ghuba ya Uajemi?

Abbas Mousavi ameashiria mwenendo wa uwajibikaji wa Iran katika kipindi cha miaka yote hii na kubainisha kwamba, kupendekeza mpango wa kupiga marufuku uvamizi, kuweko baraza la mazungumzo ya kieneo na mpango wa Ubunifu wa Amani wa Hormuz ni miongoni mwa juhudi za Iran za kuelekea kupatikana ushirikiano katika eneo.

Viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, visiwa vitatu vya Iran vya Bumusa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa ni maeneo yasiyotenganishika na ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Aidha Abbas Mousavi amesema kuwa, radiamali ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kuhusiana na hatua ya Iran ya kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni "kichekesho cha kihistoria" na kuongeza kwamba, mataifa ambayo yalifanya kila yawezalo kukwamisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA eti sasa yanajitokeza na kulalamikia hatua za zilizochukuliwa na Iran katika uwanja huo ambazo kimsingi zinaendana na sheria.