Kiongozi Muadhamu: Muamala wa Karne kamwe hautazaa matunda
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pendekezo la Marekani lililopewa jina la 'Muamala wa Karne' katu halitazaa matunda kwa Rehema za Mwenyezi Mungu.
Katika ujumbe uliotumwa kwenye ukurasa rasmi wa Twitter, Ayatullah Ali Khemenei amesema, "kwa mshangao mkubwa kwa wanasiasa wa Marekani, sera ovu na ya kishetani ya Wamarekani kwa Palestina-hicho kinachoitwa #Muamala wa Karne- kamwe hauwezi kuzaa matunda yoyote kwa Rehema za Allah."
Katika ujumbe huo na huku akikosoa vikali pendekezo la Marekani la kutaka kuyahudishwa Quds Tukufu iwe mikononi mwa Mayahudi, Kiongozi Muadhamu amesema wazo hilo ni la kipumbavu na lisilokuwa na mantiki yoyote.
Ayatullah Ali Khemenei amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina kamwe haiwezi kusahaulika na bila shaka mataifa ya Kiislamu yatasisima kidete kuhakikisha kuwa ndoto za Muamala wa Karne hazifikiwi.
Wakati huohuo, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu ameutaja Muamala wa Karne kama mpango wa fedheha uliojaa hadaa ya karne ambao bila shaka utasambaratika.
Ali Akbar Velayati amesema kadhia ya Palestina ndilo suala muhimu zaidi hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu, na Waislamu wote kote duniani wana jukumu la kuwaunga mkono Wapalestina kwa kutumia njia mbalimbali kama za kiroho, vyombo vya habari, diplomasia na hata kupitia mikusanyiko na mijumuiko ya kuzifahamisha jamii kuhusu kadhia hiyo muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.