Hatima ya Syria iko mikononi mwa wananchi wake
(last modified Thu, 28 Apr 2016 03:52:26 GMT )
Apr 28, 2016 03:52 UTC
  •  Hatima ya Syria iko mikononi mwa wananchi wake

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, wananchi wa Syria tu ndio wanaopaswa kuainisha mustakbali wa nchi yao na kwamba, hakuna mtu kutoka nje mwenye haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Dakta Ali Akbar Velayati ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kiistratijia cha Halamashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, mustakbali wa Syria unapaswa kuachwa katika mikono ya wananchi wa nchi hiyo bila ya kuingiliwa na mtu kutoka nje. Akizungumza hapa mjini Tehran Jumatano ya jana na ujumbe wa viongozi wa vyama na kaumu za Syria, Dakta Velayati amesema kama ninavyomnukuu: 'Miaka miwili iliyopita, Rais Bashar al-Assad alichaguliwa kuiongoza tena nchi hiyo kwa kipindi cha miaka saba na sisi tunaamini kuwa, anapaswa kuendelea kuingoza nchi hiyo mpaka muhula wake utakapomalizika.'

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa ameongeza kuwa, mara chungu nzima Iran imetangaza kuwa, Marekani na nchi nyingine yoyote hata za Mashariki ya Kati suala la nani awe Rais wa Syria ni jambo ambalo haliwahusu, kwani hii ni haki ya wananchi wa nchi hiyo kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Dakta Velayati amewapongeza wananchi wa Syria kutokana na kusimama kwao kidete mbele ya wavamizi na watu ambao wana uhusiano na madola ya kigeni na kueleza kwamba, jambo hilo linapaswa kupongezwa.

Tags