Rais Rouhani asisitiza kuwa JCPOA itabakia hai kwa ushirikiano
(last modified Sun, 01 Mar 2020 03:09:24 GMT )
Mar 01, 2020 03:09 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza kuwa JCPOA itabakia hai kwa ushirikiano

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yataendelea kuwepo na kubakia hai madhali kutakuwepo na ushirikiano wa pande zote husika.

Rais Rouhani alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin na kuongeza kuwa, "madhali tunastafidi na makubaliano hayo ya JCPOA, tutaendelea kufungamana na kutekeleza wajibu wetu."

Ameeleza bayana kuwa, Tehran inaamini kuwa makubaliano hayo ya JCPOA yana maslahi kwa eneo na dunia nzima kwa ujumla. 

Marekani ilijiondoa kinyume cha sheria katika makubaliano hayo mnamo Mei 8 mwaka 2018, huku nchi za Ulaya zikifeli kuchukua hatua za kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran katika mapatano hayo; jambo ambalo liliilazimisha Tehran kupunguza uwajibikaji wake hatua kwa hatua kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Kwengineko katika mazungumzo yake ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia, Rais Rouhani ametoa mwito wa kutekelezwa makubaliano ya mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria ya Astana.

Askari wa Syria mkoani Idlib, ngome ya mwisho wa magenge ya kigaidi

Dakta Rouhani amesema makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa haraka iwezekanavyo kwa shabaha ya kurejesha amani katika eneo la Asia Magharibi.

Amesema kile ambacho kinashuhudiwa hivi sasa katika mkoa wa Idlib huko kaskazini mwa Syria hakikubaliki na kubainisha kuwa, dunia haipaswi kuruhusu hali ya eneo hilo ambalo lingali chini ya udhibiti wa magenge ya kigaidi itumike na Marekani kama kisingizio cha kuivamia Syria na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

 

Tags