Marais Rouhani na Museveni wataka kuimarishwa uhusiano wa Iran na Uganda
Rais Hassan Rouhani ameutaja uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uganda kuwa mzuri na uliojengeka katika misingi ya heshima, na kusisitiza kuwa Iran iko tayari kuboresha uhusiano wa pande mbili na nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika nyuga zote.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumanne katika mazungumzo yake ya simu na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na kuongeza kuwa, "tuko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Uganda kwa kutumia fursa zote zilizopo katika mkondo wa kuimarisha uhusiano wa kirafiki."
Kadhalika Dakta Rouhani ameashiria kuhusu janga la Corona na taathira zake katika nchi za duniani na kueleza bayana kuwa, nchi zote zinapaswa kushirikiana dhidi ya janga hili la kimataifa, sambamba na kusimama kidete dhidi ya baadhi ya nchi zinazoendelea kuchukua hatua zilizo kinyume cha sheria.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, "kwa bahati mbaya, licha ya hali ngumu iliyosababishwa na mlipuko wa virusi vya Corona, lakini tunaendelea kuiona Marekani ikishadidisha vikwazo vyake haramu dhidi ya taifa la Iran; wameenda mbali zaidi na kukanyaga sheria na kanuni za kimataifa kwa kuzuia kufikishwa nchini dawa na misaada ya kibinadamu."

Kwa upande wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ameashiria kuhusu hatua hizo za uhasama na zilizo kinyume cha sheria za Marekani na kusema kuwa, "tunaamini kuwa, katika hali ngumu ya sasa, uhusiano wa kiutu ni jambo la dharura, kutangamana kwa amani kunapaswa kupigwa jeki na mizozo yote inapaswa kutatuliwa kwa njia za kisiasa."
Kadhalika ameutaja uhusiano wa Iran na Uganda kuwa wa udugu na urafiki na kubainisha kuwa, kuna umuhimu wa kuimarisha uhusiano huo wa pande mbili katika nyuga zote.