Waliopona ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran wakaribia 92,000
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran ametangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa zaidi ya 91,836 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata afueni na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran alisema hayo leo Ijumaa katika kikao cha kila siku na waandishi habari na huku akigusia kugunduliwa watu wapya 2,102 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia sasa watu 116,635 wamethibitishwa kupata ugonjwa wa COVID-19 humu nchini.
Kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 48 wa COVID-19 nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,902 wameshafariki dunia kwa ugonjwa huo humu nchini.
Daktari Jahanpour amesema hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko katika orodha ya nchi tano ambazo zina idadi kubwa ya waliopona COVID-19 duniani. Aidha amesema kwa ujumla vipimo 658,604 vya COVID-19 vimechukuliwa nchini Iran.
Hivi sasa watu walioambukizwa COVID-19 duniani ni zaidi ya milioni 4.5 ambapo mingoni mwao zaidi ya laki tatu wamefariki dunia. Aidha karibu wagonjwa milioni 1.7 wa COVID-19 duniani wamepata afueni na kuruhusiwa kuenda nyumbani baada ya matibabu hospitalini.
Hivi sasa Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa idadi kubwa ya walioambukizwa na kufariki dunia kutokana na COVID-19.