Salami: Uwezo mkubwa wa jeshi la Iran umewakosesha maadui hamu ya vita
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema utayarifu na uwezo mkubwa wa vikosi vya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimewafanya maadui wa taifa hili wakose kuwa na hata ndoto ya kuingia katika makabiliano ya kijeshi na Iran.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH alisema hayo jana Jumapili katika marasimu ya kumuarifisha mkuu mpya wa makao makuu ya Tharallah ya IRGC na kuongeza kuwa, uwezo wa kujihami Iran na nguvu kubwa za kijeshi za taifa hili zimemfanya adui aachane na propaganda za kuanzisha vita dhidi ya Iran kwa shabaha ya kujikweza tu kisiasa.
Amesisitiza kuwa, vikosi vya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viko katika kilele cha utayarifu na vitajibu chokochoko zozote za maadui kwa kasi ya juu kabisa.
Meja Jenerali Salami amebainisha kuwa, "upepo wa Mapinduzi ya Kiislamu umevuma na kuenea katika kona zote za dunia na hata katika jamii ya Marekani. Hata hivyo ni muhali kuona mfungamano wa moja kwa moja baina ya Mapinduzi ya Kiislamu na yale yanayojiri katika ulimwengu wa Magharibi."
Ameashiria kuhusu maandamano yanayoendelea kushuhudiwa nchini Marekani ya kupinga ubaguzi wa rangi wa kimfumo na kushinikiza kufanyika mageuzi ambapo ameeleza bayana kuwa, "kuchomwa moto bendera ya Marekani ni nembo ya kuonesha moyo wa mapamabano dhidi ya dhulma, na hilo linafanyika hivi sasa nchini Marekani. Hili kwa hakika limepata ilhamu kutoka katika moyo wa jihadi dhidi ya ubeberu wa Marekani na limeenea duniani kote."
Kadhalika Kamanda Mkuu wa SEPAH amebainisha kwamba, kusimama kidete taifa la Iran kumewafanya maadui wa taifa hili waendelee kudhalilika na kupata vipigo mtawalia.