Watu zaidi ya 177,000 walioambukizwa COVID-19 nchini Iran wapona
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran ametangaza kuwa, hadi hivi sasa waathirika 177,000 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Bi. Sima Sadat Lari Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran ametangaza hayo leo Ijumaa katika kikao cha kila siku na waandishi habari na kuongeza kuwa wagonjwa wapya 2,628 wa COVID-19 wamegundulika Iran katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita kufikia leo adhuhuri.
Bi. Sadat Lari amesema baina ya kesi mpya za maambukizi zilizoripotiwa, 1,356 wamelazwa hospitaliani na waliosalia wamepata matibabu bila kulazwa na kwamba kwa ujumla watu walioambukizwa COVID-19 nchini Iran ni 217,724.
Hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 109 wa corona nchini katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo adhuhuri na kusema kuwa, hadi sasa watu 10,239 wameaga dunia kwa COVID-19 hapa nchini.
Idadi jumla ya walioambukizwa COVID-19 duniani hadi kufikia Ijumaa ilikuwa takribani milioni 9.62 na waliopoteza maisha ni zaidi ya 490,000
Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo vya corona ambapo hadi kufikia leo watu zaidi ya milioni 2.4 walikuwa wameambukizwa COVID-19 na wengine wasiopungua 126,000 wamepoteza maisha.