Iran, Korea Kusini zasaini mikataba 19 ya ushirikiano
Iran na Korea Kusini leo zimetiliana saini mikataba 19 ya kuimarisha uhusiano katika nyanja mbali mbali.
Mikataba hiyo imetiwa saini katika kikao kilichohudhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Iran na Rais Pare Geun-hye wa Korea Kusini aliyeko safarini hapa Tehran.
Mikataba hiyo ni kuhusu sekta za nishati, uchukuzi, vyanzo vya maji, bandari, sayansi, elimu, afya, bima, benki na forodha.
Akizungumza baada ya kutiwa siani mikataba hiyo, Rais Rouhani amesema, kuna mazingira mazuri ya uwekezaji nchini Iran. Aidha Rais Rouhani ametoa wito wa kuwepo Amani katika Peninsula ya Korea na kusema Iran inapinga utengenezwaji wa silaha za maangamizi ya umati. Ameongeza kuwa Iran na Korea Kusini ziko tayari kuongeza kiwango cha biashara kutoka cha hivi sasa cha dola bilioni sita hadi bilioni 18.
Rais Park Geun-hye ni rais wa kwanza wa Korea Kusini kuitembelea Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika safari yake hii Rais huyo anaongoza ujumbe wa watu zaidi ya 200 wanaojishughulisha na masuala ya kiuchumi kutoka mashirika tofauti ya serikali na sekta binafsi.