Chanjo ya corona ya Iran imefanyiwa majaribio kwa mwanadamu
Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa chanjo ya corona ya Iran sasa inaendelea kufanyiwa majaribio katika mwili wa mwandamu.
Akizungumza Jumatano na waandishi habari mjini Tehran kuhusu mchakato wa kutengenezwa chanjo ya corona nchini, Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki amesema: "Mashirika ya Kiirani ambayo yana msingi wa kielimu (knowledge-based), yamepita hatua kadhaa za majaribio ya chanjo ya corona katika mwili wa mwanadamu."
Namaki amesema dunia ingali iko mbioni kutengeneza chanjo ya corona na kuongeza kuwa, bado kuna shaka kuhusu muda wa kinga itakayotolewa na chanjo ya corona iwe ni ya Iran au ya nchi nyingine yoyote. Kwa msingi huo amesisitiza kuhusu kuendelea kuzingatiwa kanuni za kiafya za kuzuia kuenea corona.

Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshiriki katika vikao vya Shirika la Afya Duniani na iwapo chanjo ya corona itapatikana sehemu nyingine duniani Iran pia itaweza kuitumia.
Waziri Namaki pia amesema takwimu za corona nchini Iran zinaonyesha kuwa, Iran haifichi chochote na inatoa taarifa sahihi na za ukweli. Hali kadhalika Waziri wa Afya wa Iran amesema idadi kubwa ya wahajiri Waafghani nchini Iran ambao hawana vibali rasmi vya kuishi Iran wanapata matibabu ya bure.