Aug 25, 2020 11:58 UTC
  • Salehi: Wakala wa IAEA unapaswa kufanya kazi zake kwa uhuru

Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unapaswa kufanya kazi zake kwa uhuru na kusisitiza kuwa Iran haiko tayari kutekeleza masuala ambayo yako nje ya ahadi zake kimataifa.

Dk Ali Akbar Salehi amesema hayo leo Jumanne wakati alipozungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, mazungumzo ya pande mbili za Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia yameenda vizuri na imekubaliwa kwamba IAEA ifanye masuala yake kwa uhuru na kiutaalamu na Iran nayo iendelee kutekeleza vizuri ahadi zake kimataifa.

Salehi aidha amesema, hatua ya Grossi ya kuitembelea Tehran hivi sasa mefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Iran na IAEA na ameelezea matumaini yake kwamba ushirikiano wa pande hizi mbili utazidi kuwa mzuri siku baada ya siku.

Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI)

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi, amesema, wakala wa IAEA hauburuzwi na nchi yoyote ingawa amekiri kwamba wakala huo uko chini ya mashinikizo.

Amesema, wakala huo umesimama imara kukabiliana na mashinikizo ya kisiasa kadiri unavyoweza na hautoruhusu mashinikizo hayo yaathiri kazi zake. Amesisitiza kuwa, kamwe hatoruhusu baadhi ya watu wautumie vibaya wakala huo kwa manufaa yao binafsi.

Amma kuhusiana na mradi wa nyuklia ya Saudi Arabia, Mkurugenzi Mkuu huyo wa IAEA amesema, imeamuliwa kwamba shughuli za nyuklia za Saudi Arabia ziwekwe chini ya uangalizi wa wakala huo.

Tags