Zaidi ya tani 3 za mihadarati zakamatwa kusini mashariki mwa Iran
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi la mkoa wa Sistan na Baluchistan huko kusini mashariki mwa Iran ametangaza habari ya kukamatwa zaidi ya tani tatu za madawa ya kulevya mkoani humo.
Brigedia Jenerali Ahmad Taheri amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, jana usiku maafisa wa kulinda usalama wa Iran walipambana na genge moja la magendo ya mihadarati wakati lilipokuwa katika harakati za kuhamisha madawa hayo. Genge hilo limekamatwa katika eneo la Mirjave la mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran.
Ameongeza kuwa, wafanya magendo hao ya mihadarati walipoona wameshazingirwa na maafisa wa polisi wa Iran, walianza kuwafyatulia risas ili wapate fursa ya kukimbia. Hata hivyo walijibiwa kwa mashambulizi makali na jeshi la polisi la Iran. Wahalifu hao walilazimika kuacha shehena ya madawa hayo ya kulevya na kukimbilia milimani na kwenye maeneo yaliyo magumu sana kupita.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi la Mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran vile vile amesema, mhalifu mmoja ameshindwa kukimbia na hivyo kutiwa mbaroni. Kiujumla tani 3 na kilo 365 za madawa ya kulevya zimekamatwa kwenye operesheni hiyo.
Brigedia Jenerali Taheri amesema, juhudi zinaendelea za kuwatia mbaroni wahalifu wengine waliokimbia hasa kutokana na kwamba mmoja wao yuko mikononi mwa polisi hivi sasa.
Licha ya kuweko chini ya vikwazo na mashinikizo ya kila aina, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaongoza katika vita dhidi ya mihadarati na madawa ya kulevya. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Iran imefanikiwa kukamata tani 950 za madawa ya kulevya kikiwa ni kiwango cha juu zaidi duniani.