Nchi za Ulaya zimeshindwa kutumiza ahadi zao kwa Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, nchi za Ulaya zimeonyesha wazi kuwa hazina uwezo wa kuondoa vikwazo dhidi ya Iran.
Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani kuwa nchi za Ulaya zitaiondolea vikwazo Iran katika fremu ya JCPOA, na kwamba vikwazo vya silaha vitaendelea hadi mwaka 2023, na kusema maamuzi ya Umoja wa Ulaya yanahusu umoja huo. Akizungumza na waandishi habari leo Jumatatu asubuhi mjini Tehran, Khatibzadeh ameongeza kuwa, Ujerumani na nchi zingine za Ulaya zinafahamu kuwa, kwa mujibu wa azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zinatakiwa kuiondolea Iran vikwazo vya silaha na hviyo hatua yoyote nyingine ni kinyume cha azimio hilo. Amesema nchi za Ulaya hadi sasa zimeshindwa kutumiza ahadi zao za kuiondolea Iran vikwazo katika fremu ya JCPOA na kuongeza kuwa nchi hizo za Ulaya hata zimeshindwa kutekeleza kikamilifu mfumo wa mabadilishano ya kifedha na Iran unaojulikana kama INSTEX.
Kwingineko katika kikao hicho, Khatibzadeh amesema Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umekuwa ukifuata mkondo potovu kwa miaka kadhaa sasa.

Akiashiria madai ya UAE kuhusu umiliki wa visiwa vitatu vya Iran na pia mpango wa nchi hiyo wa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ujenzi wa bomba la mafuta katika Ghuba ya Uajemi, Khatibzadeh amesema: "Kwa kutegemea msingi wa ujirani mwema, Iran itajaribu kuirekebisha nchi inayofanya makosa katika eneo."
Khatibzadeh amesema visiwa vitatu vya Iran katika Ghuba ya Uajemi, ambavyo UAE imekuwa ikidai ni vyake, bila shaka ni milki ya Iran na hivyo taarifa zinazotolewa haziwezi kuathiri mamlaka ya Iran juu ya visiwa hivyo.
Hivi karibuni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa UAE alidai mamlaka na umiliki wa nchi yake kwa visiwa vitatu vya Bumussa, Tomb Kubwa na Ndogo ambavyo kwa mujibu wa nyaraka za kihistoria za kuaminika visiwa hivyo ni sehemu ya ardhi ya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unaelekea kuangamia na unataka kuwavuta wengine wakati huu wa kuporomoka kwake. Ameelezea matumaini yake kuwa UAE haitaingia katika mtego wa utawala huo unaoagamia.