Rouhani: Taifa la Iran halitarajii chochote kutoka Marekani isipokuwa uadui
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria miongo mtawalia ya uadui wa Marekani kwa taifa la Iran na kusema: Taifa la Iran halitarajii chochote kutoka Marekani isipokuwa uadui.
Rais Hassan Rouhani ameeleza kuwa wananchi wa Iran hawatarajii kuziona zile nchi ambazo bila kukusudia zinaunga mkono vikwazo vya Marekani zikishiriki katika vitendo visivyo vya kibinadamu vya Marekani.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamati ya Serikali ya Uratibu wa Masuala ya Uchumi hapa Tehhran. Rais Rouhani ameashiria mapambano na muqawama wa taifa la Iran dhidi ya uadui wa Marekani na kuongeza kuwa, katika siku zijazo ukubwa wa vita vya kiuchumi vya kulazimishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia utawekwa wazi kikamilifu kwa wananchi sawa kabisa kama ilivyowekwa kwa uwazi zaidi vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Baath dhidi ya wananchi wa Iran miaka kadhaa baada ya kumalizika vita hivyo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameashiria hatua chanya zilizotekelezwa na vyombo husika ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Idara za Sheria na Benki Kuu kwa ajili ya kufanikisha haki za taifa la Iran na kutaka kuzidishwa na kupanuliwa jitihada hizo ili kukomboa akiba ya fedha za kigeni za nchi hii zilizozuiwa.