Iran yawataka Wamarekani watekeleze kivitendo maneno yao
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria jinsi Marekani inavyoendelea kutoa mapendekezo chapwa na ya kipuuzi ya kudai kutaka kuisaidia Tehran na amewaambia viongozi wa White House watekeleze kivitendo matamshi yanayotolewa na vinywa vyao.
Juzi Jumanne, Morgan Ortagus, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alidai katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba eti Washington ina wasiwasi na maambukizi ya kirusi cha corona nchini Iran na kudai kuwa White House iko tayari kusaidia kwa masharti yake ya mwezi Februari mwaka huu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana alimjibu Ortagus kupitia mtandao huo huo wa kijamii wa Twitter kwa kusema, Marekani acheni kuzua fedha za Iran katika nchi za Korea Kusini, Iraq na Japan kwani fedha hizo ni mali ya Iran na zinahitajika kwa ajili ya kukabiliana na wimbi la maambukizi ya corona na kununulia dawa na chakula.
Bw. Khatibzadeh amesema, suala ni jepesi na liko wazi kwamba viongozi wa Marekani acheni kuzuia fedha za Iran huko Korea Kusini, ziacheni zitumie kanali ya Uswisi kufika nchini Iran kwa ajili ya matumizi ya kimsingi kabisa ya kibinadamu.
Licha ya wimbi la ugonjwa wa COVID-19 kuenea duniani nzima, lakini Marekani imeshadidisha vikwazo vyake dhidi ya wananchi wa Iran kiasi kwamba mashirika ya madawa yanashindwa kufanya muamala wowote wa vifaa vya tiba na matibabu na Iran, halafu hao hao viongozi wa Marekani wanajifanya eti wana wasiwasi na kuenea ugonjwa wa corona nchini Iran.
Kabla ya hapo, Waziri wa Afya wa Iran alikuwa amewaandikia barua tofauti Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani na Mkuu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF akiitaka jamii ya kimataifa ikabiliane na vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa na viongozi wa Marekani dhidi ya wananchi wa Iran.