Khatibzadeh: Watawala wa Marekani wamepata pigo la kihistoria mkabala na Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa watawala wa Marekani wamepata pigo la kihistoria mbele ya Iran na kusisitiza kuwa, muda si mrefu viongozi hao wa Marekani watakiri rasmi kushindwa kwao.
Saeed Khatibzadeh amesisitiza kuwa, kushindwa kwa Marekani kuko wazi kikamilifu na kuongeza kuwa, Marekani imetumia uwezo wake wote kutoa pigo kwa Iran lakini Tehran haijatoa mwanya hata kidogo kwa kwa nchi hiyo wa kujihisi kuwa imeshinda.
Khatib Zadeh ameashiria pia vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran katika sekta ya dawa na matibabu na kueleza kuwa: Vikwazo vya madawa dhidi ya Iran ni jinai dhidi ya ubinadamu. Amesema mashirika na taasisi zote husika nchini Iran zinafanya kazi kwa uwezo wao wote ili kuzalisha dawa zinazohitajika kwa matumizi ya ndani.
Kuhusu hatua ya Marekani ya kuziwekea vikwazo benki 18 hapa nchini pia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa: Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran zaidi ni vita vya kisaikolojia na viongozi wa Marekani wenyewe wanajua kwamba hakuna anayeamini maneno yao kwa propaganda kama hizo.
Saeed Khatibzadeh pia ameashiria dharau na matusi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa wananchi na Iran na akasema: Nyenendo za Trump katika siasa za kimataifa ni mbaya sana kwa kadiri kwamba hazina mfano, na utamaduni na mila za Kiirani haziruhusu kujibu kejeli na matusi hayo kwa utovu wa adabu na matusi mfano wake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa matusi ya Trump dhidi ya wananchi wa Iran yametolewa kutokana na hofu na woga wa kiongozi huyo.