Bunge la Iran: Lugha za kufarakanisha za Erdogan zinashangaza na hazikubaliki
(last modified Mon, 14 Dec 2020 02:56:11 GMT )
Dec 14, 2020 02:56 UTC
  • Bunge la Iran: Lugha za kufarakanisha za Erdogan zinashangaza na hazikubaliki

Wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kusisitiza kwamba, wanategemea kutoka kwa Rais wa Uturuki ujirani mwema na kufanyika juhudi za kuweko umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu na uletaji amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi na kutangaza kuwa, lugha za kufarakanisha za Erdogan zinashangaza na katu hazikubaliki.

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 10 Disemba, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alisoma beti za mashairi katika sherehe za ushindi wa eneo la Nagorno-Karabakh mjini Baku Azerbaijan zilizohusiana na Mto Aras ambazo zilionekana zinachochea fikra za kujitenga baadhi ya maeneo ya Iran.

Balozi wa Uturuki mjini Tehran Ijumaa aliitwa katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran na kutakiwa Ankara itoe majibu ya haraka na ya wazi kuhusu beti hizo alizosoma Erdogan katika sherehe hizo.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

 

Katika taarifa yao hapo jana Jumapili, wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kulaani matamshi hayo ya ufitinishaji ya Rais wa Uturuki wamebainisha kwamba, waislamu wote ni umma mmoja na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina jukumu la kuhakikisha kwamba, katika sera zake kuu inazingatia umoja na mshikamano wa mataifa ya Kiislamu.

Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki usiku wa kuamkia jana alimpigia simu waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dk Mohammad Javad Zarif na kumuhakikishia kwamba Ankara inalipa umuhimu mkubwa suala la kuwa na uhusiano mzuri, wa kiurafiki na wa kiudugu na Tehran na kwamba, Rais Erdogan anaheshimu haki ya kujitawala taifa na ardhi yote ya Iran na wala hakuwa na taarifa kuhusu hisia kali ambazo zingeliweza kujitokeza kupitia beti za shairi zilizosomwa.