Dec 22, 2020 03:39 UTC
  • Zarif: Nchi za Ulaya zimekiuka wajibu wao katika JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema data za miamala ya kibiashara baina ya nchi hii na Ulaya kati ya mwaka 2014 na 2019 zinaonesha wazi kuwa nchi tatu za Ulaya washiriki wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA zilikiuka wajibu wao wa kisheria.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, ambapo pia ameashiria juu masuala kadhaa yaliyojadiliwa baina yake na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zinazounda kundi la 4+1.

Dakta Zarif amebainisha kuwa, miongoni mwa mambo yaliyogusiwa katika kikao hicho cha jana cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 4+1 linaoundwa na Ufaransa, Uingereza, Russia na China pamoja na Ujerumani, ni muhula kwa nchi tatu za Ulaya kuinusuru JCPOA; mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na Umoja wa Ulaya kati ya mwaka 2014 na 2019 yanayoonyesha kuwa EU na nchi tatu wanachama wake zilikanyaga majukumu yao; na nchi hizo tatu za Ulaya pamoja na Marekani zinabeba dhima kwa madhara zilizowasababishia wananchi wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, ni kitu kisichoyumkinika kuyajadili upya mapatano hayo ya kimataifa, na kwamba nchi za kidemokrasia hazipaswi kuiagiza Tehran ikiuke azimio la Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 4+1

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 4+1 katika kikao hicho kisicho rasmi cha jana pamoja na Josep Borell, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya walisisitiza katika taraifa waliyoitoa mwishoni mwa mkutano huo juu ya kufungamana na suala la kuyalinda mapatano ya JCPOA na kueleza kuwa: azimio nambari 2231 linapaswa kuendelea kutekelezwa kikamilifu. 

Aidha Mawaziri hao wa Mambo ya Nje wa Iran na kundi la 4+1 kwa mara nyingine tena wameeleza kusikitishwa sana na  hatua ya Marekani ya kujitoa kwenye mapatano hayo.   

 

Tags