Waziri wa Ulinzi wa Iran: Ushahidi unaonesha kuwa Israel ilimuua shahidi Fakhrizadeh
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuna ushahidi wa kutosha na wenye mashiko unaoonesha kuwa utawala haramu wa Israel ulihusika na mauaji ya kigaidi dhidi ya mwanasayansi bingwa wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu, Mohsen Fakhrizadeh.
Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo katika barua aliyowaandikia leo Jumatano mawaziri wenzake wa ulinzi wa nchi zaidi ya 60 duniani, ambapo amesisitiza kuwa Tehran ina haki ya kulipiza kisasi cha damu ya msomi huyo mashuhuri wa Iran.
Brigedia Jenerali Hatami ameashiria katika barua hiyo mafanikio ya Dakta Fakhrizadeh katika uga wa sayansi na utafiti, hususan uzalishaji wa zana za kupambana na ugaidi. Ameitaka jamii ya kimataifa ikomeshe undumakuwili katika vita dhidi ya ugaidi wa kiserikali, na ilaani kitendo hicho haramu, cha jinai na kisicho cha kibinadamu cha kuuawa kigaidi Dakta Fakhrizadeh.
Katika barua hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Iran ameashiria juu ya kuhusika moja kwa moja vyombo vya kiintelijensia na hususan vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mauaji ya wanasayansi wa Iran na kueleza bayana kuwa: Kuna ushahidi wenye mashiko kuhusu nafasi ya Israel katika mauaji haya (ya Shahidi Fakhrizadeh).
Amesisitiza kuwa taifa hili lina kila haki ya kulipiza kisasi dhidi ya jinai hiyo. Kwengineko katika barua hiyo, Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa wahanga wakuu wa ugaidi duniani, kwani imepoteza raia wake zaidi ya 17,000 wakiwemo maafisa wa ngazi za juu, katika vitendo vya ugaidi ndani ya miongo minne iliyopita.
Dakta Mohsen Fakhrizadeh, aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Uvumbuzi la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi Novemba 27 katika shambulio la kigaidi viungani mwa mji mkuu, Tehran.