Iran kuendelea na mazoezi ya kijeshi
Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Hussein Dehqan amesema Jamhuri ya Kiislamu haioni kizingiti chochote katika kufanya mazoezi ndani ya maji yake katika Ghuba ya Uajemi.
Akizungumza Jumamosi, ameongeza kuwa, wale wanaokuja katika eneo la Ghuba ya Uajemi kutoka umbali wa maelfu ya kilomita na kudai kuleta amani katika eneo wafahamu kuwa uwepo wao ni chanzo cha ukosefu wa usalama.
Dehqan amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kulinda maeneo yake ya anga, nchi kavu na baharini na haitakubali kitendo chochote cha kuhujumiwa.
Kauli ya Brigedia Jenerali Dehqan inakuja siku chache tu baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kusema kuwa Iran inapaswa kuonyesha uwezo wake mkubwa wa kijeshi mbele ya vikosi vya Marekani katika Ghuba ya Uajemi.
Brigedia Jenerali Dehqan amebaini kuwa Marekani na Saudi Arabia zinajaribu kuvuruga usalama wa eneo na kuandaa mazingira ya kuongeza vikosi vya Marekani na madola mengine ya kigeni katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kisingizio kuwa Iran inavuruga usalama katika hali ambayo ni wao ndio wanaovuruga usalama huo. Hivi karibuni mjumbe mmoja wa Bunge la Marekani, Congress, aliwasilisha muswada dhidi ya Iran kwa madai kuwa eti mazoezi ya kijeshi ya Iran katika Ghuba ya Uajemi ni kinyume cha sheria za kimataifa
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami. Aidha Jeshi la Iran hufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa ajili ya kubaini uwezo wa vikosi vyake na pia kufanyia majaribio zana mpya za kivita. Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.