Iran na Umoja wa Mataifa zajadili mgogoro wa Yemen mjini Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66622-iran_na_umoja_wa_mataifa_zajadili_mgogoro_wa_yemen_mjini_tehran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono kikamilifu jitihada za Umoja wa Mataifa za kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 08, 2021 12:26 UTC
  • Iran na Umoja wa Mataifa zajadili mgogoro wa Yemen mjini Tehran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono kikamilifu jitihada za Umoja wa Mataifa za kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo Jumatatu katika mkutano wake na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen, Martin Griffiths, ambaye yuko hapa mjini Tehran.

Dakta Zarif ameashiria matatizo wanayokabiliana nayo wananchi wa Yemen kutokana na vita na mzingiro wa kiuchumi na kueleza bayana kuwa, mgogoro wa Yemen unaweza tu kupatiwa ufumbuzi kupitia suluhisho la kisiasa, na wala si vita vya kulazimishwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kusaidia kwa njia na hali yoyote ile juhudi za UN za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen ambao ndio mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu hivi sasa duniani.

Kwa upande wake Martin Griffiths, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ameashiria juhudi za Iran za kujaribu kurejesha amani na utulivu nchini Yemen na kusema kuwa, Tehran ina nafasi muhimu katika kadhia ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Wajumbe wa UN na Iran wakijadili mgogoro wa Yemen hapa Tehran

Amesema mgogoro wa Yemen unaweza kufumbuliwa iwapo njia tatu zilizopendekezwa na umoja huo zitafuatwa; mosi ikiwa ni usitishaji vita, pili msaada wa kiuchumi kwa Wayemen na tatu kurejelewa mazungumzo ya kisiasa katika nchi hiyo maskini.

Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, utawala haramu wa Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi zingine kadhaa hadi sasa imeshindwa kufikia malengo yake batili tangu iivamie kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande mwaka 2015.