Mapinduzi ya Kiislamu; chimbuko la mwamko katika Ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66748-mapinduzi_ya_kiislamu_chimbuko_la_mwamko_katika_ulimwengu_wa_kiislamu
Jumatano ya juzi tarehe 10 Februari ilisadifiana na kuanza mwaka wa 43 uhai wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2021 23:08 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu; chimbuko la mwamko katika Ulimwengu wa Kiislamu

Jumatano ya juzi tarehe 10 Februari ilisadifiana na kuanza mwaka wa 43 uhai wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Katika kipindi cha miaka 42 iliyopita, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuwa na taathira chanya kwa mataifa ya eneo na duniani kwa ujumla, na hivyo kuzitia kihoro na kiwewe tawala za kibeberu ulimwenguni. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana, madola ya kibeberu yawe ni yale ya Magharibi au Mashariki yameweka katika ajenda zao mikakati ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Hata hivyo licha ya mibinyo, ukwamishaji mambo na kuwawekea mazingira magumu wafuasi na waungaji mkono wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nchi za Asia Magharibi na ulimwenguni kwa ujumla, lakini ukweli wa mambo unaonyesha kuwa, mapinduzi haya yangali yanachanja mbuga na kusonga mbele katika njia yake yaliyoichagua huku waungaji mkono wake katika kona mbalimbali duniani wakiwa nayo bega kwa bega katika safari hii na wakiendelea kuyasaidia na kuyaunga mkono.

Maandamano ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzii ya Kiislamu kutokana na hofu ya kuenea virusi vya corona mwaka huu yalifanya kwa mtindo wa aina yake wa pikipiki na magari

 

Katika uwanja huo, Hussein Usbaliev mweledi wa masuala ya kisiasa na mwananadharia wa Kygyzstan anasema: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakiwa moja ya matukio muhimu katika historia ya leo, yameendelea kuwa nukta ya matumaini kwa Waislamu na wanyonge. Usbaliev anasisitiza kuwa, hapana shaka kwamba, moyo imara, thabiti na wa kijihadi wa wananchi wa Iran katika mustakabali utakuwa pia na mafanikio yasiyo na kifani kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umma mmoja, na hii leo Iran imegeuka na kuwa kizingizi na ngome kubwa na imara isiyopenyeka mbele ya ugaidi wa kimataifa ambapo kuhusiana na suala la vita na mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na kupunguza hatari ya makundi ya kigaidi katika eneo hili na ulimwengu kwa ujumla, kwa hakika mataifa yote ya dunia ni wadaiwa wa Iran katika hili.

Bi Farhat Asif, Mkuu waTaasisi ya Pakistan inayoshughulika na masuala ya amani na sera za kigeni amesema kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ilikuwa harakati ya ndani ambayo haikuwa na uungaji mkono wowote kutoka nje ambayo kwa hakika imeyachorea Ramani ya Njia mataifa mengine ya dunia inayoonyesha kuwa, ili kufikia malengo yao matukufu njia pekee ni kusimama kidete na kuendesha mapambano.

Maoni na mitazamo inayotolewa na wataalamu na wananadharia wa nchi mbalimbali inaonyesha taathira ya kweli ya Mapinduzi ya Kiislamu yaliyopata ushindi mwaka 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhurii ya Kiislamu ya Iran.

Imam Ruhullah Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu

 

Ukweli halisi wa mambo ni kuwa, mapinduzi haya yameleta Mwamko wa Kiislamu kwa mataifa yote ya dunia. Kimsingi ni kuwa, kwa upande mmoja Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameweka wazi sura halisi ya viongozi wa Kiarabu wenye fikra mgando katika eneo la Ghuba ya Uajemi mbele ya macho ya wananchi wa eneo hili na kwa upande mwingine, mapinduzi haya yamechora bayana na wazi njia kwa mataifa ya Kiislamu na hata yasiyokuwa ya Kiislamu kwa ajili ya kurejea katika Uislamu.

Kiasi kwamba, katika miaka ya baada ya ushindi wenye fakhari wa Mapinduzi ya Kiislamu, kumeibuka wimbi kubwa la vijana wengi katika Ulimwengu wa Magharibi la kuipenda na kuikimbilia dini tukufu ya Kiislamu. Kwa maneno mengine ni kuwa, kumechipua mmea wa matumaini baina ya Waislamu. Huko nyuma dini ilikuwa ikizungumziwa kama ni jambo la historia ambalo muda wa matumizi yake umekwisha, na hivi ndivyo vijana walivyokuwa wakielezwa. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hali ya mambo ilibadilika.

Ayatullah Sayyid Ali khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

 

Kwa mfano, licha ya propaganda kubwa na za mtawalia za mfumo wa kilahidi wa Kikomonisti, dhidi ya dini hususan Uislamu katika Jamhuri za Asia ya Kati na Caucasia, Mapinduzi ya Kislamu ya Iran yalikuwa yameandaa mazingira ya kurejea mataifa ya eneo hilo katika dini tukufu ya Kiislamu kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, na ikawa imethibitishia walimwengu juu ya kutokuwa sahihi mifumo ya kilahidi.

Katika miaka ya baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti na kupata mamlaka ya kujitawala Jamhuri za Asia ya Kati na Caucasia pia taathira za Mapinduzi ya kiislamu kwa mataifa ya maeneo hayo ilikuwa kubwa mno. Kutokana na kuwa na utamaduni wa pamoja, dini na madhehebu, ustaarabu na historia kubwa baina ya Iran na Jamhuri za Asia ya Kati na Caucasia, Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kuwa na taathira muhimu na ya kukubalika katika uga wa utambulisho, dini na ustaarabu kwa mataifa ya maeneo hayo.