Iran: Tutaendelea kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Qatar jana alionana na Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS mjini Doha na kusisitiza kuwa Tehran itaendelea kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Hamid Reza Dehqani ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, ameonana na Ismail Hania mjini Doha akiwa pamoja na mabalozi wa Russia, Uturuki na Afrika Kusini.
Katika mazungumzo hayo, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amewaeleza mabalozi wa nchi hzo nne hali halisi kuhusu mabadiliko na maafikiano yaliyofikiwa baina ya makundi ya Palestina.
Dehqani ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafurahi sana kuona kuna umoja na mshikamano baina ya Wapalestina na inaliunga mkono jambo hilo.
Katika siku za hivi karibuni, makundi mbalimbali ya Palestina yamelipa umuhimu suala la kuimarisha umoja na mshikamano baina yao kwa ajili ya kukabiliana na utawala dhalimu wa Kizayuni. Makundi ya Palestina yameafikiana kuitisha uchaguzi wa Bunge baada ya miaka mingi ya kutokuwa kitu kimoja.
Hadi hivi sasa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesema mara chungu nzima kwamba wako pamoja na taifa la Palestina na wanamapambano wa taifa hilo hasa wa Ukanda wa Ghaza ambao wanaendesha mapambano ya kishujaa kukabiliana na utawala dhalimu wa Israel.