Zarif: Marekani haina haki ya kurejea JCPOA hadi pale itakapotekeleza majukumu yake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Marekani haina haki ya kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hadi pale itakapotekeleza majukumu yake.
Zarif ameyasema hayo Jumatatu mjini Tehran katika kikao cha Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran). Katika kikao hicho, Zarif amesema Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vienna, Austria ulimkabidhi barua Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossi kumfahamisha kuhusu uamuzi wa Iran wa kusitisha hatua za kujitolea za kutekeleza Protokali Ziada ya wakala huo. Kwa mujibu wa protokali hiyo IAEA ilikuwa na uwezo wa kufanya ukaguzi katika vituo vya nyuklia vya Iran nje ya ratiba ya kawaida.
Zarif amesema kufuatia uamuzi huo wa Iran mkurugenzi mkuu wa IAEA alitembelea Iran ili kujadili kuhusu njia za kuendelezwa ushirikiano wa Iran na IAEA . Amefafanua kuwa, katika safari ya Grossi hapa Tehran, alifahamishwa kuwa, kamera za IAEA zilizo katika vituo vya nyuklia vya Iran zinaweza kuendeleza kufanya kazi lakini taarifa za kamera hizo zitakabidhiwa tu IAEA iwapo nchi za Magharibi zitaondoa vikwazo katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Zarif aidha amesema kwa mujibu wa mapatano ya Iran na IAEA , iwapo hakutakua na muafaka katika kipindi hicho cha miezi mitatu, basi taarifa za kamera hizo zitafutwa.
Katika kikao chake na wabunge, Zarif amewakabidhi taarifa za hivi karibuni kuhusu Bodi ya Magavana wa IAEA na kubainisha kuwa, iwapo bodi hiyo itapitisha azimio ambalo ni haribifu kwa Iran, basi Iran itatoa jibu kali.
Zarif amesisitiza kuwa, Marekani haina haki ya kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hadi pale itakapotekeleza majukumu yake