Zarif amjibu Sherman: Hakuna mazungumzo mengine kuhusu JCPOA
-
Muhammad Javad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya Wendy R. Sherman anayetazamiwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kuhusu suala la kufanyika mazungumzo mengine ya nyuklia na Iran akisema: Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayawezi kuzungumziwa tena.
Katika ujumbe wake wa Twitter, Muhammad Javad Zarif ameashiria madai yaliyotolewa na Wendy Sherman aliyesema hali ya eneo la Magharibi mwa Asia imebadilika katika mwaka huu wa 2021 na kuna udharura wa kufanyika mazungumzo mapya na Iran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kutilia maanani hali hiyo, na kuandika: Iwapo mwaka 2021 si sawa na mwaka 2015 (mwaka wa kusainiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA), basi pia hali ya sasa si sawa na ya mwaka 1945 wakati wa kupasishwa haki ya kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kwa kutilia maanani mabadiliko ya hali ya mwaka huu wa 2021 ikilinganishwa na mwaka 1945, kuna udharura wa kufanyiwa marekebisho hati ya Umoja wa Mataifa na kufutwa haki ya kura ya veto ambayo mara nyingi hutumiwa vibaya na Marekani.
Muhammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayahitaji tena mazungumzo na ameitaka Marekani itekeleze makubaliano hayo.
Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalifikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1 linalojumuisha nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani, na yakaanza kutekelezwa Januari mwaka 2016.
Hata hivyo rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alikiuka sheria za kimataifa na kuiondoa nchi yake katika makubaliano hayo hapo tarehe 8 Mei mwaka 2018. Trump alitangaza tena vikwazo dhidi ya Iran baada ya kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano hayo.