Iran yautaka Umoja wa Ulaya uache vitisho
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezikosoa nchi za Ulaya kwa kutochukua hatua za kivitendo za kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015.
Ameongeza kuwa mazungumzo na kuheshimiana pande mbili pasina kuwepo vitisho na mashinikizo ndio njia bora zaidi ya kuondoa mkwamo uliopi.
Rais Rouhani ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland ambapo amesema ni Iran peke yake inayochukua hatua za kulinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambayo iliyatia saini na kundi la 5+1 ambazo ni China, Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani.
Rais wa Iran ametahadahrisha kuwa hali ya sasa ya upande mmoja kufungamana na mapatano hayo haiwezi kuendelea. Aidha amesema sera ya Marekani ya 'mashinikizo ya juu kabisa' imefeli na kuongeza kuwa, Iran iko tayari kusitisha hatua ilizochukua za kuacha kutekeleza kwa muda majukumu yake ya JCPOA iwapo tu Marekani itaondoa vikwazo na kusitisha sera zake za vitisho na mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei mwaka 2018 aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump alikanyaga sheria za kimataifa na kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA kisha akaanzisha tena vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.