Khatibzadeh: Uhusiano wa Iran na Marekani unategemea kuondolewa vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i67658-khatibzadeh_uhusiano_wa_iran_na_marekani_unategemea_kuondolewa_vikwazo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema uhusiano wa Iran na Marekani utategemea kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 08, 2021 07:44 UTC
  • Khatibzadeh: Uhusiano wa Iran na Marekani unategemea kuondolewa vikwazo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema uhusiano wa Iran na Marekani utategemea kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran.

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran Saeed Khatibzadeh amesema kuwa kadhia ya Iran na Marekani haihusu kutuma ishara chanya bali inahusu utekelezwaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuondolewa vikwazo. Amesema hatua hizo hazihitaji ishara bali kinachohitajika ni vitendo na hilo liko wazi.

Aidha Khatizadeh amesema Iran haina mawasiliano yoyote ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja na Marekani kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA au masuala mengine. Amesema Iran imekuwa ikifanya mazungumzo na nchi zilizosalia katika JCPOA ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani lakini haijawa na mazungumzo yoyote na Marekani.

Kwingineko, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amebainisha wasi wasi wa Iran kuhusu mgogoro wa Yemen hasa kutokana na kuwa mamilioni ya Wayemen sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji. Amesema Iran imekuwa ikisisitiza kuwa kunapaswa kuwa na usitishwaji vita Yemen na mzingiro wa nchi hiyo uhitimishwe. Aidha amesema Saudia inapaswa kusitisha vita vyake haribifu na visivyo na mlingano dhidi ya Yemen na kwamba njia pekee ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo ni mchakato wa kisiasa.