Kamanda: Vijana wa Iran watatoa jibu kali kwa maadui
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaonya maadui kuwa tishio lolote dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu kali kutoka kwa vijana wa nchi hii.
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Hussein Khanzadi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu na kuongeza kuwa: "Majeshi mawili ya majini, yaani Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), yamewazuia maadui kufika katika mipaka ya majini ya Iran." Ameongeza kuwa maadui wanafahamu kuwa tishio lolote litakabiliwa na jibu kali na lenye maangamizi la vijana wa Iran.
Akizungumza wakati wa mkutano na makamanda wa majeshi yote mawili ya majini ya Iran, Admeri Khanzadi amesema usalama umeimarishwa katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormoz na Bahari ya Oman kutokana na uwepo wenye nguvu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa, ushirikiano wa majeshi haya mawili ni muhimu katika kuangamiza njama zote za maadui kutoka nje ya eneo na kudumisha usalama.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa uwezo wake wa kijeshi ni kwa ajili ya kujihami na ni kwa maslahi ya amani na usalama wa eneo.