Nukta kuu za uwezo wa kiulinzi wa Iran katika kujibu vitisho
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i67694-nukta_kuu_za_uwezo_wa_kiulinzi_wa_iran_katika_kujibu_vitisho
Utawala wa Kizayuni unatoa vitisho na madai dhidi ya Iran kutokana na kukata kwake tamaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 09, 2021 08:16 UTC
  • Nukta kuu za uwezo wa kiulinzi wa Iran katika kujibu vitisho

Utawala wa Kizayuni unatoa vitisho na madai dhidi ya Iran kutokana na kukata kwake tamaa.

Brigedia Jenerali Amir Hatami Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku akiashiria katika kikao kilichofanyika siku ya Jumapili vitisho vya karibuni vya viongozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ameeleza kuwa, wakati mwingine viongozi wa utawala huo hutoa madai yasiyo na msingi na kulitisha taifa shupavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; jambo ambalo linabainisha wazi  kukata tamaa viongozi hao wapenda vita wa utawala wa Kizayuni. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Iran alisema katika miaka ya huko nyuma ambapo viongozi wa utawala huo walikuwa wakifanya makosa makubwa kuwa: Utawala wa Kizayuni si adui wetu namba moja, na wala hauwezi kulinganishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na wao wanalifahamu vizuri hilo. Kama hawafahamu basi wanapasa kujua kwamba iwapo watakosea kidogo tu tutaitokomeza kabisa Tel Aviv na Haifa.   

Marekani na Wazayuni wamekuwa wakitoa vitisho dhidi ya Iran tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Brigedia Hussein Dehqan Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika Masuala ya Kiulinzi anasema kuhusu matamshi na vitisho hivyo kwamba: Mtu anayekusudia kushambulia na akawa ana uwezo wa kutoa pigo dhidi ya adui yake huwa hatangazi nia yake, lakini anapopiga makelele na kupayukapayuka bila kuchukua hatua yoyote huwa anataka kustafidi na mbinu hiyo kwa lengo la kufikia maslahi yake ya kisiasa.  

Hussein Dehqan, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika Masuala ya Kiulinzi 

Kwa mujibu wa nadharia za kijeshi, hakuna mtu anayeingia vitani bila ya kwanza kuwa na uhakika na mambo mawili. Kwanza awe na uhakika wa kuibuka na ushindi vitani; na pili aweze kuvidhibiti vita hivyo na awe na uwezo wa kuvihitmisha wakati wowote anapotaka. 

Ukitupia jicho matukio ya kieneo utaona kuwa, mlingano wa kistratejia wa kijeshi katika eneo la Asia Magharibi umebadilika. Tovuti ya habari za masuala ya usalama ya DEBKA File yenye mfungamano na utawala wa Kizayuni huko nyuma ilikiri kuhusu uwezo wa makombora wa Iran na kuandika: Kinyume na mahesabu mabaya ya weledi wa Magharibi; si Marekani wala Israel iliyo na uwezo wa kukabiliana na makombora ya Iran.  

Hivi sasa uwezo wa Iran wa kumlenga adui bila kukosea umethibitika, na kujaribiwa tena uwezo huu ni kosa lisiloweza kufidiwa. Mashambulizi ya makombora ya Iran ya mwezi Januari mwaka jana yaliyotekelezwa katika kambi za kijeshi za Marekani huko Ain Asad nchini Iraq katika kujibu shambulio la kigaidi la droni za Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad lililowaua shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al Muhandes Naibu Mkuu wa Kikosi cha al Hashdu Shaabi na wanajihadi wengine kadhaa waliokuwa nao yamewadhihirishia maadui nguvu na uwezo ilionao Iran wa kujibu hujuma na mashambulizi dhidi yake.

Shambulio la Iran katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ain Asad nchini Iraq  

Nukta nyinine muhimu kuhusu uwezo wa Iran wa kukabiliana na vitisho ni nguvu laini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa nguvu za kiulinzi zina vipengee na nukta muhimu kadhaa; na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo hii imejiimarisha katika sekta zote za kiulinzi. Iran inastafidi na uwezo wake huo kwa ajili ya kudumisha amani na uthabiti na kuilinda nchi. Taaba'n kama alivyoashiria Brigedia Jenerali Amir Hatami; utawala wa Kizayuni mara kwa mara unapayuka na kuropoka kupita kiasi lengo likiwa ni kudhihirisha kuwa upo katika nafasi nzuri kijeshi. Ni dhahir shahir kuwa, Israel ipo katika eneo kupitia vitendo vyake vya kuibua mivutano na migogoro ya kieneo, kutekeleza mauaji ya kigaidi, kutoa vitisho na kuanzisha vita. Hata hivyo viongozi wanaopenda kujitanua wa utawala huo wanapasa kutambua kuwa, ushari na vitendo vyao vya kichokozi vitakabiliwa na jibu kali na zito.