Iran itakuwa mzalishaji mkubwa wa chanjo
Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, hivi karibuni Iran itakuwa mzalishaji mkubwa wa chanjo ya COVID-19 duniani.
Daktari Saeed Namaki, Waziri wa Afya wa Iran ameyasema hayo leo Jumanne na kuongeza kuwa hivi sasa Iran imeshaweka msingi wa kujitengenezea chanjo ya corona.
Daktari Namaki ameongeza kuwa: "Katika msimu wa machipuo wa mwaka ujao (1400 Hijria Shamsia unaoanza Machi 21), Taasisi ya Pasteur ya Iran itaanza kuzalisha chanjo, nayo chanjo ya Shirika la Barakat inatayarishwa na pia mashirika mengine kadhaa yamepiga hatua na yako mbioni kuunda chanjo."
Waziri wa Afya wa Iran amesema kuna uhaba wa chanjo duniani kote na hata chanjo zikipatikana bado hakutakuwa na sindano za kutosha za kuwadunga watu chanjo hiyo. Aidha amesema kwa sasa Iran inaagiza chanjo kutoka nje hadi pale itakapoanza kujitengenezea chanjo.
Hali kadhalika Daktari Namaki amesema hivi karibuni chanjo laki nne za corona zilizotengenezwa India zitaingia hapa nchini.
Hivi karibuni Alireza Raisi, Naibu Waziri wa Afya wa Iran alisema mtandao wa afya wa nchi hii una uwezo wa kuwachanja watu milioni 20 katika kipindi cha mwezi mmoja.
Alisema kuna vituo vya afya 2,500 mijini na vijijini ambavyo vina mawasiliano na hospitali, zahanati na vituo vikubwa vya afya vya Iran, hivyo hakuna wasiwasi wa kukwama kampeni ya kutoa chanjo.