Iran: Ni sisi tu undio tuliotekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Wed, 10 Mar 2021 07:14:28 GMT )
Mar 10, 2021 07:14 UTC
  • Iran: Ni sisi tu undio tuliotekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia jinsi nchi za Ulaya na Marekani zilivyoshindwa kutekeleza mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, ni Iran pekee ndiyo iliyotekeleza makubaliano hayo ya kimataifa.

Dk Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana katika mtandao wa kijamii Twitter na kuongeza kuwa, Marekani na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa, zinapaswa kuheshimu mapatano hayo na si kukwepa majukumu yao kwa visingizio hivi na vile. Amesema, JCPOA ni mpango kamili wa pamoja wa utekelezaji uliofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 ikiwemo Marekani, hivyo ni wajibu kwa pande zote kuutekeleza ndipo utakuwa na maana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, herufi "J" katika mapatano ya JCPOA ina maana ya mpango wa pamoja, hivyo madai mapya ya Marekani ya kutaka kuwa na mpango mwingine wa pamoja usio wa JCPOA hayana maana.

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Jana wabunge 140 wa Marekani walimuandikia barua Antony Blinken, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo wakitaka kufikiwa makubaliano mapya ya pamoja bila ya wabunge hao kujali kwamba ni Marekani ndiyo iliyojitoa katika mapatano ya JCPOA ambayo yenyewe maana yake ni Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji.

Tarehe 8 Mei 2018, Marekani ilijitoa kijeuri katika mapatano ya JCPOA na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo. Nchi za Ulaya ziliahidi kufidia hasara ilizosababishiwa Iran na hatua hiyo ya Marekani. Hata hivyo nchi hizo za Ulaya si tu zimeshindwa kufidia chochote, lakini zimekataa pia kutekeleza ahadi zao ndani ya JCPOA. Iran ilisubiri kwa muda wa mwaka mzima kabla ya kuchukua hatua za kujihami na kulinda haki zake ndani ya mapatano hayo.

Tags