Rais Rouhani: Taifa la Iran limeibuka mshindi katika vita vya irada
Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa kuibuka mshindi taifa la Iran katika vita vya irada kumewafanya watawala wa Ikulu ya White House wakiri mara kadhaa kushindwa kwa vita na mashinikizo yao ya juu kabisa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Shahidi na uzinduzi wa miradi ya taifa ya Taasisi ya Shahidi, ambapo sambamba na kuashiria mpango wa maadui wa kutaka kuilazimisha Iran isalimu amri mbele ya matakwa yao haramu amesema: Katika vita hivi vya irada, taifa la Iran limepata ushindi.
Rais Rouhani ameongeza kuwa, taifa la Iran limechukua hatua ambazo leo hii zimewafanya watawala wapya wa White House wakiri kila mara kwamba vita na mashinikizo ya juu kabisa yamepelekea kushindwa serikali ya Marekani; na kwa maana nyingine ni kwamba taifa la Iran limepata ushindi mkubwa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza pia kwamba: "Kwa upande wa kisiasa, kiakhlaqi na kisheria pia tumepata ushindi mkubwa na wenye kung'ara."
Kwa mujibu wa Rais Rouhani, maadui walitaka kuchukua hatua zitakazopelekea kuporomoka kwa mfumo wa utawala, lakini kutokana na moyo wa kujitolea wa wananchi wa taifa hili adhimu na imara la Kiislamu leo hii mfumo wa Kiislamu una nguvu na uwezo zaidi ya ulivyokuwa miaka mitatu nyuma.
Katika hotuba yake hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia siku ya kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW na akaeleza kwamba, inapasa wananchi wote wawe wabebaji wa mwenge wa akhlaqi njema zenye kuvutia na zilizojaa nasaha na mawaidha bora za Bwana Mtume SAW.../