Iran: Vikwazo vya upande mmoja vimewazuia mamilioni kupata chanjo ya COVID-19
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameshiriki katika kampeni ya kimataifa ya "Ni Kwa Pamoja Tu" ya kuhakikisha chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 zinapatikana kwa wote na popote pale duniani na kusema, vikwazo vya upande mmoja na vilivyo kinyume cha sheria vimewazuia mamilioni kupata chanjo ya COVID-19.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, Majid Takht-Ravanchi siku ya Ijumaa aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kusema ni kwa ushirikiano wa kimataifa tu ndio inawezekana kuangamiza janga la COVID-19 na huku akizihutubu nchi ambazo zinawekea mataifa mengine vikwazo amesema: "Sitisheni mara moja vikwazo vilivyo kinyume cha sheria ili kuokoa maisha ya watu."
Kampeni ya kuhakikisha wote wanapata chanjo ya COVID-19 ilizinduliwa Alhamisi kwa njia ya video na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye amesema mwaka mmoja wa janga la Corona umesababisha wimbi la machungu. Aliongeza kuwa, "Virusi vimeua zaidi ya watu milioni 2.5 na kuacha mamilioni na madhara ya muda mrefu ya kiafya. Familia na uchumi vinaserereka. Hivi sasa kwa ahadi hii ya chanjo, tunaona nuru."

Vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya mataifa mengine hujumuisha bidhaa za kimsingi na hata dawa na vifaa vya tiba na hivyo kusababisha matatizo mengi kwa watu ambao nchi zao zimelengwa na vikwazo hivyo vya Marekani hasa wanaougua magonjwa sugu kama saratani na COVID-19.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif alikosoa vikali sera zilizojaa uhasama za Marekani katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 na kusema dunia haiwezi kukaa kimya tena mbele ya ugaidi wa kiuchumi na ugaidi wa kitiba wa Marekani.