Rouhani: Vikwazo dhidi ya taifa la Iran ni hatua isiyo ya kibinadamu
-
Rais Hassan Rouhani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuendelezwa vikwazo dhidi ya taifa la Iran ni hatua isiyo ya kibinadamu.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana katika kikao cha kamati za kitaalamu za Kamisheni ya Taifa ya Kupambana na Corona. Amesema kuwa, kupata dawa na chanjo ni miongoni mwa haki za kimsingi kabisa za wanadamu za nchi zote za dunia lakini taifa la Iran linanyimwa haki hiyo; jambo ambalo ni dhulma kubwa na hatua isiyo ya kibinadamu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali iliyopita ya Marekani ndiyo iliyoanzisha vikwazo na vita vya kiuchumi dhidi ya taifa la Iran na kwamba, serikali ya sasa ya nchi hiyo inaendeleza vita hivyo. Amesisitiza kuwa, taarifa zinaonyesha kuwa, licha ya madai yanayotolewa kwamba hakuna kizuizi chochote cha kutumwa dawa na chanjo ya corona nchini Iran, lakini kuna matatizo mengi katika njia ya kufikisha chanjo ya kigeni hapa nchini, na hatua hiyo isiyo ya kibinadamu inahatarisha afya na uzima wa wananchi.
Vilevile ameashiria juhudi kubwa na mafanikio yaliyopatikana katika utengenezaji chanjo ya corona hapa nchini na kusema, kuna matumaini ya kudhibitiwa kikamilifu maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 hapa nchini mwaka huu baada ya kukamilishwa mchakato wa kutoa chanjo kwa umma.