Bunge la Iran lapinga kuondolewa vikwazo taifa hili hatua kwa hatua
Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imepinga pendekezo la kuondolewa vikwazo taifa hili hatua kwa hatua.
Taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha wazi cha Wabunge wa Iran leo Jumapili imebainisha kuwa, sera thabiti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuzitaka pande zote husika za makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuiondolewa nchi hii vikwazo vyote kwa mkupuo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, vikwazo vyote dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa, na hilo lithibitishwe na Bunge la Iran kabla ya Marekani kuruhusiwa kurejea katika mapatano hayo ya kimataifa. Marekani ilijiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2018.
Taarifa ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu imeongeza kuwa, Bunge la Iran litaendelea kutekeleza Sheria ya Mpango wa Kistratajia wa Kukabiliana na Vikwazo iliyopasishwa Disemba mwaka jana, hadi pale vikwazo vyote vya kidhalimu vilivyowekewa nchi hii katika utawala wa Donald Trump na mtangulizi wake Barack Obama viondolewa kikamilifu.

Mapema leo pia, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliashiria mkutano wa Vienna wa Kamati ya Pamoja ya JCPOA utakaofanyika Jumanne ijayo na kusema kuwa, "Tunataka Marekani kwanza itekeleze ahadi zake zote katika mapatano hayo na iondoe vikwazo vyote na kisha baada ya hapo tutabainisha msimamo wetu."
Kadhalika Wabunge wa Iran katika kikao cha wazi cha mapema leo wamekaribisha kwa mikono miwili na kupongeza mapatano ya kistratijia ya miaka 25 yaliyotiwa saini karibuni baina ya Iran na China.