Rouhani: Taifa la Zimbabwe litavishinda vikwazo vya Marekani
(last modified Mon, 19 Apr 2021 02:54:38 GMT )
Apr 19, 2021 02:54 UTC
  • Rouhani: Taifa la Zimbabwe litavishinda vikwazo vya Marekani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia ujumbe wa pongezi mwenzake wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa kwa mnasaba wa Siku ya Uhuru wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, iliyoadhimishwa jana Jumapili.

Katika ujumbe wake, Rais Rouhani ameipongeza serikali na taifa la Zimbabwe kwa ujumla kwa maadhimisho ya Siku ya Uhuru, ambayo anasisitiza kuwa ni matunda ya kusimama kidete na jitihada za miaka mingi za kupambana na ubeberu na ubaguzi wa rangi.

Dakta Rouhani amesema anaamini kuwa, miongo minne baada ya kujinyakulia uhuru kutoka kwenye makucha ya wakoloni, wananchi wa Zimbabwe kupitia mapambano na uvumilivu, watavuka salama changamoto na matokeo hasi ya vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi yao.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 18 Aprili mwaka 1980 iliyosadifiana na tarehe ya jana miaka 41 iliyopita, Zimbabwe ambayo wakati ule ilikuwa ikijulikana kwa jina la Rhodesia, ilijipatia uhuru, baada ya kukoloniwa na Uingereza kuanzia mwishoni mwa karne ya 19.

Wananchi wa Zimbabwe katika maandamano ya kulalamikia vikwazo vya kidhalimu vya US

Rais Rouhani amesema taifa la Iran liko tayari kuwapa wananchi wa Zimbabwe msaada wa aina yoyote katika njia yao ya kuhakikisha kuwa uhuru wao unadumu.

Kadhalika Dakta Rouhani amemtakia Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe afya na siha njema, sanjari na kuliombea fanaka taifa hilo la Kiafrika.