Iran: Mazungumzo ya Vienna yatasitishwa US ikiendelea kushupalia vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69792-iran_mazungumzo_ya_vienna_yatasitishwa_us_ikiendelea_kushupalia_vikwazo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mazungumzo ya Tehran na kundi la 4+1 yanayoendelea huko Vienna, Austria yatasimamishwa iwapo Marekani itaendelea kushupalia suala la kuwekewa vikwazo taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2021 03:06 UTC
  • Iran: Mazungumzo ya Vienna yatasitishwa US ikiendelea kushupalia vikwazo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mazungumzo ya Tehran na kundi la 4+1 yanayoendelea huko Vienna, Austria yatasimamishwa iwapo Marekani itaendelea kushupalia suala la kuwekewa vikwazo taifa hili.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa, Marekani inasisitiza kuendelea kuwekewa vikwazo vikali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna.

Amesema kuna tofauti nyingi zilizoibuka kati ya Iran na Marekani kwenye mazungumzo hayo na kwamba baadhi ya misimamo inayotolewa na wawakilishi wa Washington haikubaliki.

Wakati huohuo, duru za kuaminika zimeiambia Press TV kuwa, iwapo Marekani itaendelea kupinga suala la kuondolewa vikwazo vyote taifa hili, hakuna shaka kwamba Iran itasitisha mazungumzo hayo ya Vienna.

Mazungumzo ya Vienna

Maafisa wa Iran wanasisitiza kuwa, msimamo thabiti wa Tehran katika mazungumzo na kundi la 4+1 ni kuondolewa kikamilifu vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya taifa hili.

Washiriki katika mazungumzo ya Vienna wamerejea katika nchi zao kwa ajili ya mashauriano baada ya kumalizika duru nyingine ya vikao hivyo, na wanatazamiwa kukutana tena Ijumaa kuendeleza mazungumzo hayo yanayoonekana kuwa magumu.