Jun 05, 2021 12:01 UTC
  • Mgombea urais Iran: Sitounda serikali ila ambayo nina uhakika itafanya kazi

Mmoja wa wagombea katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatounda serikali ila ya watu ambao kweli watawatumikia wananchi na watawatekelezea matakwa yao kwa ukweli na udhati wa moyo.

Shirika la habari la Iran Press limetangaza hayo leo na kumnukuu Sayyid Ebrahim Raisi, mmoja wa wagombea wa uais katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Iran akitoa ahadi hizo kwenye mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya 3 ya televisheni ya Iran. Ameongeza kuwa, kushikamana na kutekeleza vilivyo miongozo ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo la dharura na kwamba sasa hivi imepatikana fursa nzuri ya kumtambua vizuri zaidi Imam Khomeini MA.

Amesema, serikali ni sehemu muhimu sana ya kuendesha nchi na kutumikia wananchi na kwamba wanasiasa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuliko watu wote wengine katika kutekeleza na kulinda miongozo ya Imam Khomeini MA na kufuata maadili mema na misimamo yake ya kisiasa.

Sayyid Ebrahim Raisi

 

Wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu nchini Iran ni Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisi, Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.

Wagombea wote nchini Iran wanapewa haki sawa kwa kuhesabiwa mpaka sekunde za kufanya kampeni katika vyombo vya habari vya taifa kama vile redio na televisheni, bila ya kupunguziwa au kuongezewa hata sekunde moja.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa 6 wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe  18 mwezi huu wa Juni, 2021.

Tags