Amir Abdollahian: Israel haina nafasi katika mustakabali wa Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71942-amir_abdollahian_israel_haina_nafasi_katika_mustakabali_wa_asia_magharibi
Hossein Amir-Abdollahian, mshauri maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema: "Utawala wa Israel hautakuwa na nafasi yoyote katika mustakabali wa eneo (la Asia Magharibi).
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jul 03, 2021 08:13 UTC
  • Amir Abdollahian: Israel haina nafasi katika mustakabali wa Asia Magharibi

Hossein Amir-Abdollahian, mshauri maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema: "Utawala wa Israel hautakuwa na nafasi yoyote katika mustakabali wa eneo (la Asia Magharibi).

Amir Abdollahian ameyasema hayo katika ujumbe alioutuma kwa njia ya Twitter na kuongeza kuwa: "Pamoja na kuwa utawala wa Tel Aviv ulishindwa katika makabiliano ya hivi karibuni na Wapalestina; kufunguliwa balozi za utawala huo ambao unawaua watoto katika Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain kunaonyesha watawala wa nchi hizo mbili hawana ufahamu sahihi kwani wamefungamanisha hatima yao na utawala wa Kizayuni."

Abdollahian aidha amesisitiza kuwa, hakuna shaka kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel hautakuwa na mustakabali; Wazayuni wanawaua pia Mayahudi na kuwateka nayara."

Hayo yanajiri wakati ambao raia wapatao 5,000 wa utawala haramu wa Israel wamepewa uraia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Tovuti ya kuvujisha uovu wa watawala wa UAE ya 'Emirates Leaks' imenukuu vyanzo vya habari vikithibitisha habari hiyo na kuripoti kuwa, Imarati imewapa Wazayuni hao uraia kwa kisingizio kuwa ni wawekezaji.

Haya yameripotiwa siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid,  kuitembelea UAE na kufungua rasmi ubalozi wa utawala huo wa Kizayuni katika mji mkuu Abu Dhabi, na pia ubalozi mdogo wa utawala huo pandikizi mjini Dubai.

Mwaka jana Umoja wa Falme za Kiarabu, Sudan, Bahrain na Morocco zilianzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel.