Iran: Israel inabeba dhima ya kutekwa wanadiplomasia wa Kiirani Lebanon
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake ndio wanaobeba dhima ya kisiasa na kisheria kuhusu hatima ya wanadiplomasia wanne wa Kiirani waliotekwa nyara nchini Lebanon mwaka 1982.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ilisema hayo jana Jumapili kwa mnasaba wa kutimia miaka 39 tangu wanadiplomasia hao wa Kiirani walipotekwa nyara.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza bayana kuwa: Utawala wa Kizayuni ulioikalia kwa mabavu Lebanon mwaka 1982, unabeba dhima ya kisheria na kisiasa ya kutekwa nyara wanadiplomasia wa Kiirani; utawala huo wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa kigaidi ndio waliohusika na kitendo hicho.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa ina ushahidi unaoonesha kuwa, wanadiplomasia wa Kiirani waliotekwa walikabidhiwa kwa jeshi la utawala haramu wa Israel na kisha wakapelekwa katika magereza ya utawala huo wa Kizayuni.
Juni 4 mwaka 1982, mwaka ambao utawala ghasibu wa Israel ulivamia ardhi ya Lebanon, wanadiplomasia wanne wa Kiirani Ahmad Motevasselian, Seyyed Mohsen Mousavi, Taqi Rastegar Moqaddam na Kazem Akhavan walitekwa na genge la watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha katika kituo kimoja cha upekuzi kaskazini mwa Lebanon.
Kwa mara nyingine tena, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kuangalia kwa makini suala la kutekwa wanadiplomasia wa Iran na utawala haramu wa Israel.