Jenerali Salami: Vita vijavyo vitaashiria mwisho wa uhai wa Israel
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameukumbusha utawala wa Kizayuni juu ya uwezo mkubwa wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika mapambano na vita vya nchi kavu na kuonya kuwa, hatua yoyote ghalati itakayopelekea kuibuka vita vipya, haitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kufutwa Israel katika uso wa dunia.
Meja Jenerali Hossein Salami alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake hapa Tehran na Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na kuongeza kuwa, jibu la hivi karibuni la Hizbullah dhidi ya Israel lilikuwa onyo kwa Waziri Mkuu mpya wa utawala huo haramu kwamba, hakuna chochote kilichobadilika katika mapambano dhidi ya Tel Aviv.
Kamanda Salami amesisitiza kuwa, uwezo mkubwa wa kijeshi wa harakati ya muqawama ya Hizbullah hususan katika makabiliano ya ardhini, utawalazimisha Wazayuni kutafuta pa kukimbilia.
Amesema wimbi kubwa la kujaribu kutoroka bila kuwepo njia za kukimbilia litawaandama Wazayuni, kutokana na mgogoro mkubwa wa kisaikolojia utakaosababishwa na kitendo cha kusambaratishwa utawala huo pandikizi.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuiunga mkono Hizbullah kwa kila namna na sio kupitia misaada na uungaji mkono wa kijeshi tu.
Meja Jenerali Salami amesema, "injini ya Hizbullah ikichemka, Wazayuni watalazimika kukimbia katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu."