Shamkhani aionya Israel; Hatima ya uvamizi ni kutimuliwa
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuuambia kuwa, sera yake ya uvamizi na ukaliaji ardhi za Wapalestina kwa mabavu itapatwa na hatima ya kufedhehesha kama iliyoipata Marekani huko Afghanistan.
Ali Shamkhani amesema hayo leo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamiii wa Twitter ambapo ameashiria kuondoka vikosi vya Marekani nchini Afghanistan na kusema: Mwisho wa uvamizi wowote ni kutimuliwa kwa fedheha.
Amesisitiza kuwa, "Hatima iliyoikumba Marekani katika nchi za Vietnam, Afghanistan na Iraq, hakuna shaka itaukumba utawala ghasibu wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi (za Wapalestina)."
Marekani licha ya kutumia zaidi ya dola trilioni 2.26 kwa mujibu wa uchunguzi wa 'Mradi wa Gharama za Vita' uliofanywa na Chuo Kikuu cha Brown tokea mwaka 2001, lakini hatimaye imelazimika kuondoka kwa madhila nchini Afghanistan.
Marekani katika wiki za hivi karibuni imekuwa ikiviondoa vikosi vyake nchini Afghanistan, huku kundi la Taliban likitangaza kumalizika kwa vita katika nchi hiyo baada ya kudhibiti taasisi zote za serikali katika mji mkuu, Kabul.