Iran yaionya Marekani; Msithubutu kuzuia meli zetu za mafuta zinazoelekea Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i74100-iran_yaionya_marekani_msithubutu_kuzuia_meli_zetu_za_mafuta_zinazoelekea_lebanon
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani haina haki wala mamlaka ya kuzuia biashara halali baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyinginezo duniani huku akiionya vikali Washington dhidi ya kuzuia meli za mafuta za nchi hii zinazoelekea Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2021 07:01 UTC
  • Iran yaionya Marekani; Msithubutu kuzuia meli zetu za mafuta zinazoelekea Lebanon

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani haina haki wala mamlaka ya kuzuia biashara halali baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyinginezo duniani huku akiionya vikali Washington dhidi ya kuzuia meli za mafuta za nchi hii zinazoelekea Lebanon.

Saeed Khatibzadeh ametoa indhari hiyo leo Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa: Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, serikali ya Iran ina haki ya kuiuzia nchi yoyote ile mafuta, na mara hii imeichagua Lebanon.

Amesema, "Marekani haipo juu ya sheria, haina haki ya kuzuia biashara halali kati ya Iran na Lebanon. Lebanon ni taifa tajiri halihitaji misaada, linaweza kukidhi mahitaji yake. Baadhi ya nchi zinapaswa kukoma kuingiza siasa katika kila jambo."

Khatibzadeh amebainisha kuwa, meli hizo za mafuta za Iran zipo njia kuelekea Lebanon na hivi sasa zinakaribia Mfereji wa Suez licha ya Marekani, Saudi Arabia na waitifaki wao kujaribu kuzizuia.

Meli ya mafuta

Hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma shehena ya mafuta kuelekea Lebanon; na Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah akaonya kuwa, uchokozi wowote utakaofanywa dhidi ya shehena hiyo utakuwa ni uchokozi dhidi ya ardhi ya Lebanon.

Tangu mwaka uliopita wa 2020 Lebanon imegubikwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kisiasa; na katika muda wote huu Marekani si tu haijatoa msaada wowote wa kutatua matatizo ya nchi hiyo, bali imetumia visingizio mbali mbali kuiwekea vikwazo Lebanon na kuwasababishia wananchi wake dhiki kubwa ya maisha.