Mtazamo wa serikali mpya ya Iran kuhusu kuhuishwa mazungumzo ya nyuklia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Ufaransa na Austria kuhusu sera za kigeni zenye mlingano, kuratibu uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Hussein Amir-Abdollahian katika mazungumzo hayo ya simu yaliyofanyika nyakati tofauti aliashiria kuhusu kuhuishwa mazungumzo ya mapatano ya JCPOA mjini Vienna na kusisitiza kuwa, "mazungumzo ya Vienna yanapaswa kudhamini maslahi na haki za Iran na pia Marekani inapaswa kusitisha mwenendo wake usio wa uwajibikaji na hali kadhalika Umoja wa Ulaya uachane na sera zake za kutotekeleza ahadi zake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kusema kuwa, msingi wa mazungumzo ya Vienna unakubalika lakini mazungumzo yanayotakikana ni yale ambayo yatapelekea vikwazo kuondolewa kivitendo na kudhaminiwa haki za Iran.
Kuhakikisha na kuthibitisha kuwa vikwazo vya Marekani vimeondolewa ni msingi mkuu katika kuhuisha mapatano ya JCPOA na hatua ya pili baada ya hapo itakuwa ni Iran kuanza tena kutekeleza ahadi zake katika JCPOA. Hizo ndizo nukta za msingi katika sera za Iran kuhusu kuhuishwa mazungumzo ya Vienna. Lakini katika duru sita za mazungumzo ya Vienna Marekani imekuwa ikisisitiza sera ya 'Hatua Mkabala wa Hatua' na hii ni sera ambayo Iran haiafiki.
Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa Marekani kama nchi ambayo ilijiondoa katika mapatano ya JCPOA ndiyo inayopaswa kuchukua hatua ya kwanza na baada ya Iran kuthibitisha kuwa Marekani inatekeleza ahadi zake baada ya kurejea katika mapatano, nayo hapo itachukua hatua na kutekeleza ahadi zake katika JCPOA. Mazungumzo yaliyopita ya Vienna kwa lengo la kuhuisha mapatano ya JCPOA wakati wa serikali iliyopita ya Iran yalifeli kutokana na Marekani kusisitiza kuhusu sera zake za upande mmoja.
Baada ya kuingia madarakani, serikali mpya nchini Iran bado hakujatangazwa tarehe ya kuanza upya mazungumzo ya Vienna ya kuhuisha JCPOA lakini pamoja na hayo serikali mpya ya Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa haitashiriki katika mazungumzo kwa ajili ya kufanya mazungumzo tu. Hivyo njia pekee ya kuhuisha mapatano ya JCPOA ni Marekani na Ulaya kutekeleza kivitendo ahadi zao katika mapatano hayo na baada ya hapo Iran iweze kuthibitisha kuwa ahadi hizo zimetekelezwa na hayo yakitimia Iran nayo itachukua hatua ya kuanza kutekeleza majukumu yake katika JCPOA ambayo ilikuwa imesitisha kutokana na ukiukwaji uliofanywa na upande wa pili.
Kama alivyosema Hussein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Ujerumani na Austria, Iran imetekeleza jukumu lake katika kuhifadhi mapatano ya JCPOA kwa subira ya kistratijia iliyokuwa nayo wakati Marekani ilipojiondoa katika mapatano hayo na pia wakati nchi za Ulaya zilikosa kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo. Kwa msingi huo sasa ni wakati wa upande wa Markani na nchi za Ulaya kuchukua hatua za kivitendo za kutekeleza ahadi zao katika JCPOA.
Iran imesisitiza kuwa itashiriki tu katika mazungumzo ambayo yatapalekea kudhaminiwa haki na maslahi ya watu wa Iran.
Inavyoelekea ni kuwa utawala wa sasa wa Marekani chini ya Rais Joe Biden unafuatilia zile zile sera zilizofeli za Trump za mashinikizo ya juu dhidi ya Iran. Kinyume na ilivyodai huko nyuma, serikali ya Biden inatumia vikwazo haramu kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Lakini kama alivyosisitiza Amir-Abdollahian, Iran haitasalimu amri mbele ya mashinikizo kama hayo.