Ulaya, Marekani zitekeleze mapatano ya nyuklia ya Iran kivitendo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i7507-ulaya_marekani_zitekeleze_mapatano_ya_nyuklia_ya_iran_kivitendo
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito kwa nchi za Ulaya na Marekani kuchukua hatua za kivitendo kuondoa vikwazo vya kibenki na kiuchumi dhidi ya Iran kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia mwaka jana kati ya Tehran na madola sita makubwa duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2016 11:28 UTC
  • Ulaya, Marekani zitekeleze mapatano ya nyuklia ya Iran kivitendo

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito kwa nchi za Ulaya na Marekani kuchukua hatua za kivitendo kuondoa vikwazo vya kibenki na kiuchumi dhidi ya Iran kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia mwaka jana kati ya Tehran na madola sita makubwa duniani.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo hapa mjini Tehran alipohutubia kikao cha waandishi habari akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Murray McCully leo Jumamosi.

Ikumbukwe kuwa Iran na kundi la nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia Julai 14, 2015 baada ya miaka miwili na nusu ya mazungumzo ya kina ya nyuklia.

Kwa mujibu wa mapatano hayo yaliyoanza kutekelezwa Januari 16 mwaka huu, vikwazo vyote vilivyohusiana na miradi ya nyuklia vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilipaswa kuondolewa.

Mkabala wa hilo Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shuguhuli zake za nyuklia. Iran imeshatekeleza ahadi zake lakini nchi za Ulaya na Marekani bado hazijatekeleza ahadi zilizotoa.

Zarif amesema hatua ya ujumbe mbalimbali wa ngazi za juu wa kisiasa wa nchi tofauti za dunia kutembelea Iran ni ishara kuwa jamii ya kimataifa inataka kushirikiana na Iran. Amesema sera za kiuadui za Marekani ni kizingiti kwa nchi mbali mbali za dunia kushirikiana na Iran.