Iran: Nchi za Magharibi zisifanye tamaa katika mazungumzo ya Vienna
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mazungumzo ya mjini Vienna yataingia kasi inayotakiwa iwapo madola ya Ulaya na Marekani yataacha tamaa na kupenda mambo yaliyo nje ya makubaliano ya JCPOA.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo Jumamosi katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov. Waziri wa mambo ya Nje wa Iran amepongeza pia misimamo sahihi na imara ya Russia kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia makubaliano yaliyofikiwa kuhusu wakati wa kufanyika mazungumzo baina ya Iran na kundi la 4+1 na kusisitiza kuwa, kasi ya mazungumzo hayo inahitaji upande wa Ulaya na Marekani kuachana na tamaa zao za kutaka vitu vilivyoko nje ya mapatano ya JCPOA, bali ziangalie mambo katika uhalisia wake.
Vile vile amesisitiza kuwa, ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nia ya kweli ya kuhakikisha pande zote zinarejea kikamilifu kwenye mapatano hayo na kwamba si sahihi hata kidogo kutilia shaka nia hiyo ya kweli ya Tehran.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza katika mazungumzo hayo ya simu kwamba kuna wajibu wa kufufuliwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema kuwa, pande zote hasa hasa Marekani zina wajibu wa kuheshimu kikamilifu ahadi zao kwenye mapatano hayo.
Vile vile amesema, nchi yake muda wote imekuwa ikitilia mkazo wajibu wa Marekani wa kuachana na vitendo vyake vya kuharibu makubaliano ya JCPOA.