Takht-Ravanchi: Vikwazo vya Marekani vinakwamisha ustawi endelevu katika nchi mbalimbali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76740-takht_ravanchi_vikwazo_vya_marekani_vinakwamisha_ustawi_endelevu_katika_nchi_mbalimbali
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vinazizuia nchi mbalimbali kupata vyanzo vya fedha na ustawi unaohitajika kwa ajili ya kutimiza malengo ya ustawi endelevu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2021 03:01 UTC
  • Takht-Ravanchi: Vikwazo vya Marekani vinakwamisha ustawi endelevu katika nchi mbalimbali

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani vinazizuia nchi mbalimbali kupata vyanzo vya fedha na ustawi unaohitajika kwa ajili ya kutimiza malengo ya ustawi endelevu.

Majid Takht-Ravanchi ambaye jana alihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana kujadili suala la kulinda amani na usalama wa kimataifa, aliashiria uraibu wa Marekani wa kuziwekea vikwazo nchi mbalimbali na kusema kuwa, utumiaji wa mabavu wa serikali ya Washington, kama vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya wananchi wa Iran, una taathira hasi na kubwa kwa maisha ya raia wa matabaka yote ya jamii. 

Takht-Ravanchi amesema kuwa, vitendo hivyo vinavyokiuka sheria ambavyo vimesababisha uhaba mkubwa wa mahijati ya msingi ya wananchi hususan dawa na vifaa vya tiba vinavyohitajika kwa ajili ya kupambana na virusi vya corona, umesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi. 

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema masuala kama umaskini, ukosefu wa usawa na uadilifu vinaweza kuwa chachu ya kushadidi migogoro na machafuko na kudhoofisha jitihada za kuimarisha amani endelevu katika nchi zinazosumbuliwa na mizozo.

Majid Takht-Ravanchi amesema kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kushikamana ipasavyo na malengo na misingi ya hati ya umoja huo na kuongeza kuwa, masuala kama umaskini na ukosefu wa usawa vinavyohusiana na masuala ya kijamii na kiuchumi vinapaswa kushughulikiwa na  taasisi husika za Umoja wa Mataifa.