Nov 11, 2021 05:00 UTC
  • Iran yaiachilia huru meli iliyokuwa imebeba mafuta ya kuibwa

Meli ya mafuta iliyokuwa inashikiliwa Iran kutokana na kuhusika katika wizi wa mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeachiliwa kufuatia hukumu ya mahakama na baada ya mafuta hayo kurejeshwa.

Mnamo Oktoba 24, meli ya mafuta inayojulikana kwa jina la MV Sothys, ilinaswa na makomando wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika Bahari ya Oman wakati Jeshi la Majini la Marekani lilipokuwa likiisindikiza baada ya kujazwa mafuta yaliyoibwa kutoka meli ya mafuta ya Iran. Jeshi la Majini la Marekani lilikuwa linalenga kuelekeza na kudhibiti mafuta hayo ya Iran yaliyoibwa lakini katika oparesheni maalumu makomando wa Iran wakafanikiwa kuzuia uharamia huo wa Marekani.

Admeli Alireza Tangsiri, Kamanda wa Kikosi cha Majini cha IRGC , ameshiriki katika hafla iliyofanyika Jumatano kuwaenzi walioshiriki katika oparesheni hiyo ya kihamasa ya kukabiliana na jeshi la utawala wa kigaidi wa Marekani ambalo lilikuwa linatekeleza uharamia. Katika hafla hiyo amebainisha namna oparesheni  hiyo ilivyofanyika na kusema Kikosi cha Majini cha IRGC  kilikuwa tayari kutekeleza oparesheni hiyo kubwa. 

Askari wa Kikosi cha Majini cha IRGC wakiwa katika makabiliano na meli ya kivita ya Marekani

Iran inakabiliwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani ambavyo havijawahi kuwekwa dhidi ya nchi  yoyote nyingine duniani lakini pamoja na kuwepo hatua hizo zilizo kinyume cha sheria, Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kuwafikishia wateja wake mafuta. 

Marekani ina historia ndefu ya kutekeleza vitendo vya uharamia dhidi ya meli za mafuta za Iran kwa kisingizio kuwa eti meli hizo zinakiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

 

Tags