Iran: Mazungumzo kuhusu Uingereza kutulipa deni letu yangali yanaendelea
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema mjini London Uingereza kwamba mazungumzo kuhusu Uingereza kuilipa Tehran deni lake la mamia ya mamilioni ya Pound, yanaendelea ingawa hadi hivi sasa mchakato na namna ya kulipwa deni hilo haijafikiwa mwafaka.
Televisheni ya al Alam imelinukuu shirika la habari la Bloomberg likiripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, katika mahojiano aliyofanyiwa mjini London, Uingereza, Naibu Waziri Ali Bagheri Kani amesema, kuna matumani deni la Pound milioni 400 sawa na dola milioni 535 za Kimarekani ambazo Uingereza inadaiwa na Iran, zitalipwa karibuni hivi. Hivi sasa nchi hizo mbili zinajadiliana juu ya mchakato na namna ya kulipwa deni hilo ambalo linatokana na mkataba wa kijeshi uliowekwa baina ya London na utawala wa zamani wa Iran miongo kadhaa iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ali Bagheri Kani ambaye pia ndiye mkuu wa timu ya mazungumzo yajayo ya Vienna amesema kuwa, suala hilo lilijadiliwa pia juzi Alkhamisi katika mazungumzo yake na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza.
Sasa hivi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yuko katika ziara ya kuzitembelea nchi mbalimbali za Ulaya kwa ajili ya kutafuta njia za kuondolewa vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Tehran. Ziara hiyo inafanyika wakati huu wa kukaribia kufanyika mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 4+1 kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Ali Bagheri Kani vile vile amekanusha madai ya kuweko uhusiano wowote baina ya kulipwa Iran deni lake hilo na suala la mfungwa mwenye uraia pacha wa Iran na Uingereza, Nazanin Zaghari-Ratcliffe, aliyeko korokoroni nchini Iran.